Swahili New Testament Bible

Matthew 11

Matthew

Return to Index

Chapter 12

1


 

  Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake.  

 

 

--

2


 

  Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, "Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato."  

 

 

--

3


 

  Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?  

 

 

--

4


 

  Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao.  

 

 

--

5


 

  Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia?  

 

 

--

6


 

  Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu*fd* kuliko Hekalu.  

 

 

--

7


 

  Kama tu mngejua maana ya maneno haya: `Nataka huruma wala si dhabihu`, hamngewahukumu watu wasio na hatia.  

 

 

--

8


 

  Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato."  

 

 

--

9


 

  Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao.  

 

 

--

10


 

  Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, "Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?" Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki.  

 

 

--

11


 

  Lakini Yesu akawaambia, "Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato?  

 

 

--

12


 

  Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato."  

 

 

--

13


 

  Kisha akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine.  

 

 

--

14


 

  Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu.  

 

 

--

15


 

  Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote,  

 

 

--

16


 

  akawaamuru wasiwaambie watu habari zake,  

 

 

--

17


 

  ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie:  

 

 

--

18


 

  "Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote.  

 

 

--

19


 

  Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani.  

 

 

--

20


 

  Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale.  

 

 

--

21


 

  Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini."  

 

 

--

22


 

  Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona.  

 

 

--

23


 

  Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, "Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?"  

 

 

--

24


 

  Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, "Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo."  

 

 

--

25


 

  Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka.  

 

 

--

26


 

  Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje?  

 

 

--

27


 

  Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi.  

 

 

--

28


 

  Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.  

 

 

--

29


 

  "Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake.  

 

 

--

30


 

  "Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.  

 

 

--

31


 

  Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.  

 

 

--

32


 

  Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao.  

 

 

--

33


 

  "Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake.  

 

 

--

34


 

  Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni.  

 

 

--

35


 

  Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya.  

 

 

--

36


 

  "Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema.  

 

 

--

37


 

  Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia."  

 

 

--

38


 

  Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako."  

 

 

--

39


 

  Naye akawajibu, "Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona.  

 

 

--

40


 

  Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha.  

 

 

--

41


 

  Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona!  

 

 

--

42


 

  Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu*fe* kuliko Solomoni.  

 

 

--

43


 

  "Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate.  

 

 

--

44


 

  Hapo hujisemea: `Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.` Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa,  

 

 

--

45


 

  huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu."  

 

 

--

46


 

  Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye.  

 

 

--

47


 

  Basi, mtu mmoja akamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe."  

 

 

--

48


 

  Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, "Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?"  

 

 

--

49


 

  Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, "Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu!  

 

 

--

50


 

  Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu."  

 

 

--

Matthew 13

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: